3333

Posted on: April 29th, 2024

Timu ya Madaktari Bingwa na Mabingwa wabobezi 35 wa Dkt Samia kutoka Hospitali za Nyanda za Juu kusini ikihusisha Hospitali za mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Songwe wameanza kutoa huduma matibabu mbalimbali kwa wananchi mkoani Ruvuma.

Akizungumza katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya madaktari bingwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songea, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abass Ahmed amewataka wananchi kujitokeza kupata matibabu kwenye kambi ya Madaktari bingwa na ubingwa bobezi wa Dkt. Samia

Kanali Ahmedi amesema lengo Serikali ni kusogeza huduma bora za  matibabu kwa wananchi ili kuimarisha afya zao na ili waweze kuendelea kulijenga taifa na kujipatia maendele yao binafsi ya kila siku.

“Niwaombe wananchi tuikimbile hii fursa ya kufikiwa na kambi hii ya madaktari bingwa kwani sina shaka kazi nzuri inayofanywa na wataalamu wetu hawa yote ni matokeo ya uwekezaji na nguvu kubwa ya Serikali katika sekta ya Afya hivyo niwahimize wananchi tujitokeze kwa wingi katika kipindi chote cha huduma hizi za kibingwa”amesema Kanali Ahmed

Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dr. Magafu Majura amesema lengo kuu ni kuwatumia mabingwa waliopo katika Hospitali na Taasisi zetu kufikisha matibabu ya ubingwa wao kwa wananchi wengi na kwa wakati mmoja

“Uwepo wa kambi hii inawapelekea wananchi kupata huduma za kibingwa kwa gharama nafuu pia matarajio yetu ni kutoa huduma wananchi zaidi ya elfu 3000 katika kipindi hiki cha kambi hii inayoanza leo tarehe 29/04/2024 hadi 3/05/2024”

Dkt Majura ametaja matibabu yatakayotolewa magonjwa ya akina mama na uzazi, huduma za magonjwa ya watoto, hudumaza kibingwa za magonjwa ya ndani kama vile kisukari, shinikizo la damu, figo na moyo, huduma za upasuaji na mifupa, huduma za macho, huduma za Afya ya akili, huduma za kinywa na meno, huduma za masikio, pua na koo, huduma za ngozi, huduma za mfumo wa chakula, huduma za moyo kwa watoto, huduma za saratani.

Pia amongezea magonjwa mengine yatakayochunguzwa ni magonjwa ya watoto,mifupa,upasuaji,macho,kinywa,meno,upasuaji wa midomo sungura,masikio,pua,koo,afya ya akili,ngozi,moyo,mfumo wa chakula na saratani.

Amesema, Wizara ya Afya na TAMISEMI inaendelea kuboresha huduma za kibingwa na ubingwa bobezi kwa kuwatumia madaktari waliopo katika Hospitali za rufaa za mikoa,kanda,taasisi na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.