MAFANIKIO YA KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA MOYO RUVUMA
Posted on: November 15th, 2025Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea, Dkt. Magafu Majura, amesema kambi ya madaktari bingwa wa moyo kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa imepokelewa kwa mwitikio mkubwa wa wananchi waliokuwa na uhitaji wa huduma za kibingwa.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya kambi hiyo, iliyofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 21 Novemba 2025, Dkt. Majura ameeleza kuwa imekuwa na manufaa makubwa si tu kwa wagonjwa, bali pia kwa madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo.
Ameeleza kuwa Kupitia ushirikiano na madaktari bingwa waliokuja kutoa huduma, watumishi wa hospitali walipata nafasi ya kujengewa uwezo na kuongeza ujuzi.
Aidha, Dkt. Majura ametoa shukurani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuimarisha sekta ya afya kupitia uboreshaji wa miundombinu, upatikanaji wa vifaa tiba, na ajira kwa watumishi wapya.
Pia, alimpongeza Mkurugenzi wa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Profesa Abeli Makubi, kwa kuruhusu madaktari bingwa kufika mkoani Ruvuma na kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Dkt. Mwanaisha Serugendo kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa ameeleza furaha yake kwa kushiriki katika utoaji wa huduma hizo. Pia ameishukuru serikali ya mkoa na wilaya pamoja na uongozi wa hospitali kwa mapokezi mazuri na ushirikiano uliowezesha kufanikisha zoezi hilo.
Dkt. Serugendo amewaasa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kuzingatia ushauri wa kitaalamu kuhusu namna ya kujikinga na magonjwa ya moyo.



