NURU YAREJEA MBINGA ZAIDI YA WAGONJWA 3,000 WATIBIWA MACHO

Posted on: May 9th, 2026


Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea kwa kushirikiana na shirika la Eye Corps kutoka Marekani, madaktari wa KCMC Moshi na CCBRT wametoa matibabu kwa wangonjwa wa macho zaidi ya 3,000 katika Halmashauri ya Mji Mbinga.

 Kliniki hiyo imeanza Aprili 27 kwa kutembelea vijiji zaidi ya 7 kufanya uchunguzi wa magonjwa ya macho na kuhitimishwa Mei 8, 2026, katika Hospitali ya Mbinga Mji.

 Mkurugenzi wa Eye Corps Tanzania, Bw. Raymond Rafael, amesema zaidi ya wagonjwa 164 wenye matatizo ya mtoto wa jicho wamefanyiwa upasuaji, huku wengine wakipatiwa dawa na miwani. Pia wanatarajia kuendelea na kambi za macho katika Mkoa wa Ruvuma mwezi Julai, Septemba na Novemba mwaka huu wa 2026. 

Aidha, ametoa shukurani kwa wataalamu kutoka Marekani, madaktari wa KCMC Moshi, CCBRT, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea pamoja na wauguzi na wataalamu wa macho wa Hospitali ya Mbinga Mji.

 Kwa upande wake, Mratibu wa zoezi hilo mkoani Ruvuma, ambaye ni Daktari Bingwa wa magonjwa ya macho Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dkt. Charles Hinjo, amesema kliniki hiyo imefanikiwa kwa kiwango kikubwa na wananchi wengi wamejitokeza kupata huduma.  

“Naishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutunganisha na wadau wanaosaidia huduma za macho kwa wananchi”. Amesema. 

Vilevile, Daktari wa macho kutoka hospitali ya Mbinga Mji, Dkt. Neema Joseph, amesema huduma hiyo imekuwa na mwitikio mkubwa na imewasaidia sana wananchi wa Mbinga na vijiji jirani. 

Mnufaika wa kliniki hiyo, Martin Kabweza, amewashukuru madaktari kwa kumsaidia kuondoa tatizo la mtoto wa jicho na sasa anaweza kuona tena. 

Naye mkazi wa Mbinga alie nufaika na huduma hiyo Agusta Milinga, ameshukuru kwa huduma bora iliyomwezesha kuona tena.