WAUGUZI WAFAWIDHI WASISITIZWA KUSIMAMIA NIDHAMU MAHALI PA KAZI.
Posted on: November 19th, 2025Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo, amewasisitiza wauguzi wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa kusimamia kikamilifu nidhamu, maadili ya kazi na mawasiliano thabiti baina ya watumishi, wagonjwa pamoja na ndugu wa wagonjwa.
Ametoa wito huo wakati akifungua kikao cha wauguzi wafawidhi wa hospitali za rufaa za mikoa nchini kilichofanyika katika ukumbi wa Songea Club mjini Songea, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed.
“Ni matumaini yangu kuwa kikao hiki kitajadili na kupanga mikakati madhubuti itakayosaidia kuimarisha mifumo ya utoaji huduma ya uuguzi na ukunga, huku tukizingatia staha na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na watoto wachanga,” alisema Bi. Makondo.
Ameeleza kuwa Serikali ina imani kubwa na wauguzi, hivyo itaendelea kuwajengea uwezo kupitia nyanja mbalimbali ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Kwa upande wake, Muuguzi Mkuu wa Serikali, Bi. Ziada Sellah, amesema mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu na ushauri wa kitaalamu kuhusu namna bora ya kuboresha huduma za uuguzi nchini.
Amebainisha kuwa kama wauguzi kipaumbele chao katika utendaji wa kazi ni kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naye Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea, Dkt. Magafu Majura, akimwakilisha Mwenyekiti wa Waganga Wafawidhi Tanzania, amewashukuru na kuwapongeza wauguzi wafawidhi na wasaidizi kwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku kwa uadilifu na kujituma na imepelekea uboreshwaji wa huduma zinazotolewa katika hospitali zetu za rufaa za mikoa siku hadi siku



