WAUGUZI WASISITIZWA UPENDO NA WELEDI KWA WAGONJWA

Posted on: May 12th, 2026


Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dkt. Victor Mhezi amewasisitiza wauguzi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi, upendo, unyenyekevu na kutumia lugha ya staha wanapowahudumia wagonjwa.

Ametoa kauli hiyo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea leo Mei 12, 2026.

 Akizungumza na wauguzi waliohudhuria maadhimisho hayo, Dkt. Victor Mhezi amesema kuwa taaluma ya uuguzi ni uti wa mgongo wa sekta ya afya na inahitaji moyo wa kujitoa. Mgonjwa anayekuja na maumivu anahitaji upendo kwanza, kisha dawa. 

Kwa upande wake Kaimu Muuguzi Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Imakulata Ndunguru amesema watu 217 wamefaidika na huduma za uchunguzi wa kiafya zilizotolewa na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea katika wiki ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani. 

Huduma hizo ni upimaji wa uzito na urefu, Saratani ya mlango wa kizazi, maambukizi ya Ukimwi,upimaji wa BP, uchangiaji wa damu, kisukari, kutoa ushauri wa Lishe bora na utoaji wa elimu ya Afya ambazo zilianza tarehe 8/5/2026 hadi tarehe 10/5/2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea.

 Lengo kuu lilikuwa kuwafikia wananchi wenye uhitaji na kutambua mchango wa wauguzi katika kutoa huduma za afya ya msingi. 

“Tumeamua kuadhimisha siku ya wauguzi kwa vitendo kwa kuwafikia wananchi moja kwa moja” amesema Ndunguru. Aidha Kati ya 217 wateja watu waligundulika kuwa na sukari, sita waligundulika kuwa na presha ya juu, wateja 123 walikuwa na uzito uliozidi na wakina mama watatu walikutwa na changamoto ya Saratani ya Mlango wa kizazi kati ya hao mmoja ameanza matibabu wawili wanaendelea na uchunguzi.