MKURUGENZI MTENDAJI WA HOSPITALI MAALUM YA TAIFA YA MAGONJWA AMBUKIZI KIBONG’OTO AMEAHIDI KUSHIRIKIANA NA UONGOZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA SONGEA.
Posted on: July 20th, 2025
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali Maalum ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi Kibong’oto, Dkt. Leonard Subi amesema wanatoa huduma za matibabu ya magonjwa Ambukizi mojawapo ni ugonjwa wa kifua kikuu bila malipo yeyote pindi mgonjwa anapopima na kugundulika kuwa ana ugonjwa wa kifua kikuu.
Ameyasema hayo baada ya kufika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea wakati akitembelea maeneo mbalimbali ya Hospitali hiyo.
Lengo la ziara ya Dkt. Subi, ni kufanya ufuatiliaji shirikishi (Supportive supervision) na kuhakikisha wagonjwa wa kifua kikuu wanapata matibabu yaliyo sahihi na kupata stahiki zao muhimu za kimatibabu ili waweze kupona na wasiweze kuambukiza watu wengine. Pia kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao na kuwaweka wananchi katika hali ya Afya njema.
Dkt. Subi ameupongeza Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea kwa kuimarisha miundombinu ya Hospitali, Ubora wa Huduma za Afya ikiwemo vipimo vya maabara hasa vya ugunduzi wa Kifua Kikuu na uwepo wa vipimo vyote muhimu vya ufuatiliaji wa wagonjwa wa kifua Kikuu Sugu.
Vilevile, Dkt. Subi ameahidi kushirikiana na Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea ikiwemo kuwajengea Uwezo wataalamu mbalimbali wa Afya katika maeneo mbalimbali ya taaluma zao hususani katika Magonjwa Ambukizi na eneo la uchunguzi wa maabara ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za Afya.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Songea Dkt. Magafu Majura ameshukuru ujio wa Dkt. Leonard Subi kwa ujumbe aliotoa Songea RRH wapo tayari kuendelea kushirikiana na Hospitali ya Kibong'oto ili kuimarisha afua za Kifua Kikuu na magonjwa Ambukizi mengine kwa ujumla ikiwemo kutoa wataalamu wake ambao watapata nafasi ya kwenda kujengewa uwezo, kujifunza na kuongeza ujuzi, ili kuongeza ubora katika utoaji wa huduma za Afya.